Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

El Niño yatishia wakazi Milioni 60 katika nchi zinazoendelea- WHO

El Niño yatishia wakazi Milioni 60 katika nchi zinazoendelea- WHO

Shirika la afya duniani, WHO na wadau wake wametoa ripoti leo ikitabiri kuwa ongezeko kubwa la dharura za kiafya kutokana na mwelekeo wa El Niño ambayo kwingineko inasababisha mvua kubwa na mafuriko na kwingineko ukame.

WHO imesema mvua kubwa zeney mafuriko zimeanza kushuhudiwa Tanzania, Kenya na Ecuador ilhali Ethiopia na Malawi hazipati mvua za kutosha na hivyo wigo wa madhara hayo utakuwa mkubwa zaidi mvua za El Niño zitakapomalizika na watu wapatao Milioni 60 katika nchi hizo wako hatarini zaidi.

Mathalani nchi hizo zinaweza kukumbwa na ukosefu mkubwa wa chakula, mlipuko wa magonjwa na kuharibika kwa miundombinu ya usambazaji wa maji.

Dokta Richard Brennan, Mkurugenzi wa WHO kitengo cha udhibiti wa dharura amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi kuwa kinachotakiwa sasa ..

(Sauti ya Dokta Brennan)

Tunahitaji kuendelea kushirikiana na serikali za kitaifa na jamii ili kuimarisha uwezo wa kukabili na majanga na tunahitaji kuendelea kufanya hivyo mwaka wote huu. WHO na wadau wake imeanza kufanya hivyo kwenye nchi kadhaa na tuko tayari kuongeza usaidizi iwapo tutaombwa na serikali.”

Mvua za El Niño ambazo tayari zimeanza mwaka jana na zinaendelea zinatabiriwa kuwa na madhara zaidi ikilinganishwa na zile za mwaka 1997-1998 ambazo nazo pia zilikuwa na madhara makubwa ya kiafya duniani ikiwemo mlipuko wa malaria, kipindupindu na homa ya bonde la ufa.