Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ugaidi nchini Somalia ni kikwazo kwa kukuza haki za binadamu

Ugaidi nchini Somalia ni kikwazo kwa kukuza haki za binadamu

Mwanasheria Mkuu wa Somalia, Ahmed Ali Dahir amesema tishio kubwa kwa haki za binadamu nchini Somalia ni mashambulizi ya kigadi dhidi ya viongozi wa serikali na raia. Priscilla Lecomte na taarifa kamili.

(Taarifa ya Priscilla)

Bwana Dahir amesema hayo leo wakati Somalia ikiangaziwa katika Kikao cha Baraza la Haki za Binadamu mjini Geneva, Uswisi, huku mafanikio ya Somalia yakimulikwa katika masuala ya haki za watu walio wachache, vijana na wanawake.

(Sauti ya Bwana Dahir)

“ Vikwazo vikubwa zaidi kwa ulinzi wa haki za Binadamu Somalia ni hali dhaifu ya usalama kutokana na ugaidi. Serikali ya Somalia imejitahidii kuhakikisha usalama wa taifa pamoja na haki za raia kujieleza huru na kuandamana. Ni changamoto kubwa hasa serikali ikijaribu kupata uwiano kati ya usalama na haki za binadamu ambazo mara nyingi ni kanuni tatanishi.”

Wakati huo huo, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Michael Keating amelaani vikali mashambulizi yaliyotokea Alhamisi mjini Mogadishu na kuua zaidi ya watu 20.