Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wataalam wa UM wasihi Ethiopia kutotumia ukatili dhidi ya waandamaji

Wataalam wa UM wasihi Ethiopia kutotumia ukatili dhidi ya waandamaji

Wataalam wa haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa leo wameisihi serikali ya Ethiopia kusitisha hatua kali zinazochukuliwa na vikosi vya usalama dhidi ya waandamanaji nchini humo, huku tayari waandamanaji zaidi ya 140 wakiwa wameuawa na wengine kufungwa.

Kwenye taarifa iliyotolewa leo, wataalam hao wameeleza kwamba maandamano hayo yameanza wiki tisa zilizopita baada ya serikali ya Ethiopia kutangaza mpango wa kupanua mipaka ya mji mkuu Addis Abeba, ambao utalazimisha maelfu ya watu wa jamii ya Oromo kufurushwa makwao, ardhi kuchukuliwa na misitu kuondolewa.

Wataalam wamekaribisha uamuzi wa serikali kusitisha kwa muda utekelezaji wa mpango huo, wakisisitiza umuhimu wa kusitisha pia ghasia dhidi ya waandamanaji.

Aidha wameiomba serikali kuachilia huru waandamanaji waliofungwa kwa madai ya ugaidi wakati ambapo walikuwa wanatekeleza haki yao ya kuandamana kwa amani.