Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lengo la dola milioni 750 kusaidia shule kwa watoto wa Syria lazima lifikiwe:Brown

Lengo la dola milioni 750 kusaidia shule kwa watoto wa Syria lazima lifikiwe:Brown

Mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa kuhusu elimu Gordon Brown ameitolea wito dunia wakiwemo wafanyabiashara kufikia lengo la dola milioni 750 katika wiki mbili zijazo ili kufadhili maeneo ya shule kwa ajili ya watoto milioni moja wakimbizi wa Syria.

Akizungumza katika kongamano la kimataifa la uchumi mjini Davos Uswisi, Bw Brown amesema tayari dola milioni 500 zimeshakusanywa na kupongeza  mchango muhimu wa biashara kwa mchango katika kukabiliana na mgogoro huo kubwa zaidi wa kibinadamu tangu mwaka 1945.

Amesema elimu ni ufunguo wa kupunguza msafara wa watu kuelekea Ulaya, kunusuru watoto kutokana na ajira ya watoto, kuwaepusha na ndoa za mapema, biashara haramu na usafirishaji wa watu na siasa za misimamo mikali na kuwapa matumaini kwa kizazi kilichopotea.

Bw brown amesema wasichana na wavulana wamesambaa Lebanon, Uturuki na Jordan, lakini wanapata matumaini kutokana na mfumo maalumu wa elimu uliogawanyika mara mbili ambao unatoa elimu kwa watoto wazawa saa za asubuhi na mchana na watoto wakimbizi wanatumia madarasa hayo hayo saa za alasiri na jioni.