Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dunia ipaze sauti kukomesha machafuko Syria: WFP

Dunia ipaze sauti kukomesha machafuko Syria: WFP

Ikiwa ni takribani miezi 60 tangu kuzuka kwa mgogoro wa Syria , Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP kwa pamoja na mashirika 100 ya misaada ya kibinadamu yametoa tamko zito leo wakitaka dunia ipaze sauti kukomesha machafuko nchini Syria ili kutoa ahueni kwa mamilioni ya raia wanaoteseka nchini humo.

Tamko hilo limetolewa mjini Roma Italia, ambapo shirika la mpango wa chakula duniani na mashirika mengine yametia saini tamko hilo ambalo pia limeeleza hatua za haraka za kuimarisha hali ya kibinadamu husuani ufikiwaji wa wahitaji nchini Syria.

Taarifa ya WFP imesema kwamba umma unaweza pia kutia saini tamko hilo kupitia mitandao ya kijamii kama vile twitter na mingineyo ambapo shirika hilo litaweka tamko hilo kupitai mitandao yake yote ya kijamii.

Kadhalika WFP imesema katika kutoa msisistizo wa ukomeshwaji wa machafuko Syria , inaandaa video maalum inayoonyesha madhila wanayokumbana nayo raia wa Syria kutokana na ghasia zinazoendelea.