Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ubia mpya kusaidia wakulima wadogo wadogo kupata masoko- WFP

Ubia mpya kusaidia wakulima wadogo wadogo kupata masoko- WFP

Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP limetangaza kuingia makubaliano ya kuwezesha wakulima wadogo wadogo katika nchi zinazoendelea kupata masoko ya mazao yao.

Mkurugenzi Mtendaji wa WFP Etharin Cousin ametangaza mpango huo leo huko Davos, Uswisi wakati wa jukwaa la uchumi duniani akisema makubaliano yanahusisha mashirika makubwa ya umma na ya kibinafsi.

Amesema kupitia mfumo wa manunuzi, PPP itakuwa rahisi kwa wakulima kupanda, kuvuna na kuuza mazao yenye ubora wa hali ya juu na hivyo kuongeza uhakika wa upatikanaji wa chakula.

Wakulima watawezeshwa kupewa siyo tu mbegu bora na pembejeo bali pia bima, usaidizi wa fedha na soko la uhakika.

Miongoi mwa mashirika yaliyotia saini makubaliano hayo ni AGRA, Bayer, GrowAfrica, WFP na Rabobank.

WFP inasema kupitia makubaliano hayo zaidi ya wakulima Milioni Moja maskini zaidi duniani wataweza kubadili kilimo chao kutoka cha kujikimu hadi cha biashara kwani watakuwa wanaingia mikataba hata kabla ya msimu wa upanzi wa mazao.

Tayari mpango huo unanufaisha wakulima huko Rwanda, Tanzania na Zambia.