Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNEP na Benki ya maendeleo ya Kiislam watia saini makubaliano ya uhifadhi wa mazingira

UNEP na Benki ya maendeleo ya Kiislam watia saini makubaliano ya uhifadhi wa mazingira

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Mazingira(UNEP) na Benki ya Maendeleo ya Kiislam IDB leo wameafikiana kushirikiana katika masuala mbalimbali yanayohusu uhifadhi wa mazingira katoka kupigia upatu maendeleo endelevu na vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Naibu mkurugenzi mtendaji wa UNEP Bw. Ibrahim Thiaw na Rais wa IDB, Dr. Ahmad Mohammad Ali al Madani wametia saini muafaka huo mjini Jeddah Saudi Arabia yaliko makao makuu ya IDB.

Makubaliano hayo yatakayodumu hadi June 2018 katika awamu ya awali yatajikita katika malengo muhimu ya mashirika hayo mawili hususani katika masuala ya mabadiliko ya tabia nchi, kilimo na usalama wa chakula, ubunifu na uchumi unaojali mazingira na ufadhili wa kiislam.

Lengo kuu la ushirika huu kwa mujibu wa mashirika hayo mawili ni kusaidia utekelezaji wa ajenda ya mwaka 2030 ya maendeleo endelevu na mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabia nchi. IDB imepanga kuongeza ufadhili wake katika malengo ya maendeleo endelevu SDG’s kufikia zaidi ya dola bilioni 150 katika miaka ijayo.