Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi ya wenye njaa CAR yaongezeka maradufu– WFP

Idadi ya wenye njaa CAR yaongezeka maradufu– WFP

Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP na wadau wake limesema kuwa nusu ya wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR wanakabiliwa na njaa ambapo, mtu mmoja kati ya sita ikiwemo, wanawake, watoto na wanaume hawana uhakika na mlo wa baadaye. John Kibego na taarifa zaidi.

 (Taarifa ya Kibego)

Katika taarifa yake ya leo, WFP imesema idadi hiyo ya wenye njaa ambyo ni karibu Milioni Mbili nukta Tano ni karibu maradufu ya idadi  ya mwaka jana, wakati huu ambapo mzozo na ukosefu wa usalama vimekwamisha upatikanaji wa chakula.

Naibu Mkurugenzi mkazi wa WFP nchini CAR Guy Adoua amesema miaka mitatu ya mzozo nchini humo imekuwa na madhara makubwa kwa wananchi na familia zao ambapo wamelamizika kuuza mali zao, kuondoa watoto wao shuleni na hata kusalia ombaomba.

Amesema wana hofu kubwa kutokana na kiwango cha njaa na ukosefu wa lishe bora nchini humo na hivyo wameomba usaidizi wa dharura wa chakula na kuweka mipango ya kuwezesha watoto kupata mlo shuleni sanjari na kukarabati miundombinu ya kijamii.