Skip to main content

M-Power yashinda tuzo ya nishati za baadaye Abu Dhabi

M-Power yashinda tuzo ya nishati za baadaye Abu Dhabi

Shirika la Off Grid Electric lenye makao makuu yake nchini Tanzania ni miongoni mwa washindi tisa wa tuzo ya Zayed Future Energy iliyotangazwa leo mjini Abu Dhabi, falme za kiarabu.

Tuzo hiyo ya dola milioni 4 inatuza watu, kampuni na shule bunifu katika nishati mbadala.

Off Grid Electric ambayo inajulikana kwa jina la M-Power inauza paneli za miyonzi ya jua Tanzania na Rwanda kwa bei nafuu na inalenga kuwapatia watu milioni moja nchini Tanzania huduma za umeme kupitia ushirikiano na serikali.

Akihutubia maadhimisho ya kutangaza washindi leo mjini Abu Dhabi, Daktari Han Seung-soo, Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu kupunguza madhara ya majanga, amesema ni muhimu kusaidia watu wanakumbwa na madhara ya mabadiliko ya tabianchi kupitia nishati mbadala.

Ameongeza kwamba vyanzo endelevu vya kuzalisha umeme vitachangia katika kutokomeza umaskini na pia kupunguza utoaji wa gesi chafuzi.