Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukosefu wa ajira watarajiwa kuongezeka 2016 na 2017- ILO

Ukosefu wa ajira watarajiwa kuongezeka 2016 na 2017- ILO

Licha ya kushuka viwango vya ukosefu wa ajira katika baadhi ya nchi zilizoendelea, ripoti mpya ya tathmini ya Shirika la Kazi Duniani, ILO imeonyesha kuwa mzozo wa ajira duniani huenda hautaisha, hususan katika nchi zinazoibuka.

Ripoti hiyo imesema kuwa kuendelea kuwepo viwango vya juu vya ukosefu wa ajira kote duniani na ajira duni katika nchi nyingi zinazoibuka na zinazoendelea, kunaathiri vibaya hali ya ajira.

Makadirio ya ukosefu wa ajira mwishoni mwa mwaka 2015 yalionyesha kuwa idadi ya watu wasio na ajira iliongezeka hadi watu milioni 197, ikiwa ni kwa kiwango cha asilimia 5.8. Idadi hiyo inatarajiwa kupanda kwa milioni mbili mwaka huu hadi milioni 199 mwaka huu, na hadi zaidi ya milioni 200 mwaka 2017.

Guy Ryder ni Mkurugenzi Mkuu wa ILO..

“Kinachotia hofu hapa, mbali na kuwa idadi hii inamaanisha kuwa sasa tuna watu milioni 27 zaidi wasio na ajira kuliko tulivyokuwa kabla ya mdodoro wa uchumi, nadhani kinachotia hofu zaidi ni makadirio ya miaka miwili ijayo ambapo takwimu zinaonyesha kuongezeka kwa ukosefu wa ajira duniani, kwa milioni 2.3 mwaka huu 2016 na kwa milioni 1.1 mwaka 2017.”

Bwana Ryder ameeleza ni kwa nini hali inaonekana kutotia matumaini hivi...

“Kutokana na ukuaji mdogo sana wa uchumi wa kimataifa, uchumi wa kimataifa hauzalishi ajira za kutosha, za kuweza kubadili mwelekeo wa kiwango cha juu cha ukosefu wa ajira duniani.”