Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Messi miongoni mwa wajumbe wa jopo la kuchagiza utekelezaji wa SDGs

Messi miongoni mwa wajumbe wa jopo la kuchagiza utekelezaji wa SDGs

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametangaza jopo la watu 17 maarufu la kuchagiza utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs yaliyopitishwa mwaka jana.

Taarifa ya msemaji wake imesema jopo hilo litaongozwa na Rais John Draman Mahama wa Ghana kwa ushirikiano na Waziri Mkuu wa Norway Erna Solberg.

Wajumbe wengine ni Bi. Graca Machel, mcheza soka maarufu na balozi mwema wa UNICEF Lionel Messi pamoja na Shakira ambaye pia ni mwimbaji na balozi mwema wa UNICEF.

Watetezi hao watatumia uelewa na uongozi wao kuchagiza utekelezaji wa malengo hayo 17 kwa kuzingatia msingi wa kuhakikisha hakuna mtu yeyote anayeachwa nyuma.

Mathalani kuona kushirikisha wadau wote katika utekelezaji na uchangishaji fedha, kuhamasisha ubia kati ya serikali , mashirika ya kiraia na sekta binafsi sambamba na kuongeza uelewa wa jinsi malengo hayo yote yanavyotegemeana.