Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashambulizi ya Boko Haram, UNHCR yahaha kusaidia waliopoteza makazi

Mashambulizi ya Boko Haram, UNHCR yahaha kusaidia waliopoteza makazi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi,  UNHCR na wadau wake wanahaha kusaidia takribani watu Laki Moja waliopoteza makazi yao kutokana na mashambulizi yaliyofanywa na Boko Haram hivi karibuni.

Wakazi hao kutoka eneo la Diffa, kusini-mashariki mwa Niger wako katika mazingira magumu kutokana na kukosa makazi, vyakula na wanahusisha pia wenyeji ambao walikuwa wanawapatia hifadhi wakimbizi kutoka Nigeria.

Msemaji wa UNHCR Geneva, Adrian Edwards amesema kwa sasa wanaelekeza misaada iliyopo kukidhi mahitaji ya dharura na linatoa wito kwa wahisani kusaidia raia hao ambao wako katika mazingira magumu.

Hata hivyo amesema usambazaji misaada kwa wanachi hao ni tatizo kwa kuwa wamesambaa tofauti na wanapokuwa kambini ambako usambazaji wa huduma unakuwa rahisi halikadhalika usalama ni wa uhakika.

UNHCR inasema inatarajia raia zaidi kukimbia makazi yao wakati wa msimu wa kiangazi katika wiki chache zijazo wakati huu ambapo jeshi la Niger nalo linatarajiwa kuanza operesheni ya kijeshi dhidi ya magaidi hao wa Boko Haram.

Mzozo kaskazini-mashariki mwa Nigeria umelazimu zaidi ya watu 220,300 kusaka hifadhi nchi jirani tangu mwaka 2013 ikiwemo Niger, Cameroon na Chad.