Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi ya wanaopoteza maisha Iraq ni kubwa-ripoti ya UM

Idadi ya wanaopoteza maisha Iraq ni kubwa-ripoti ya UM

Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa leo inaelezea kwa undani athari kubwa za vita vinavyoendelea kwa raia nchini Iraq, ikionyesha takriban raia 18,802 wameuawa na wengine 36,245 kujeruhiwa kati ya Januari Mosi 2014 na Oktoba 31 mwaka 2015.

Ripoti pia inasema watu wengine zaidi ya milioni tatu wamekuwa wakimbizi wa ndani wakiwemo watoto zaidi ya milioni moja wa umri wa kwenda shule katika kipindi hicho hihco.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyoandaliawa na mpango wa Umoja wa Mataifa Iraq, UNAMI na Ofisi ya Kamishina Mkuu wa Haki za Binadamu imetokana zaidi na ushahidi uliokusanywa toka kwa waathirika , manusura au walioshuhudia ukiukwaji wa haki za kimataifa za binadamu ikiwa ni pamoja na mahojiano na wakimbizi wa ndani.

Ripoti pia imeelezea ukatili mkubwa na mauaji ya kutisha yanayofanywa na kundi la ISIL ikiwemo ya hadharani kwa kuwapiga risasi, kuwakata vichwa, kuwauwa na mabuldoza, kuwachoma moto wakiwa hai na kwa kuwarusha watu kutoka maghorofani.