Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yaonya juu ya hatari ya watu wa Pembe ya Afrika wanaovuka bahari kuingia Yemen

UNHCR yaonya juu ya hatari ya watu wa Pembe ya Afrika wanaovuka bahari kuingia Yemen

Takwimu za karibuni za shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR kuhusu wanaowasili kwa njia ya bahari kuingia Yemen zinaonyesha licha ya mgogoro unaoendelea watu zaidi ya 92,000 waliwasili kwa boti 2015.

UNHCR inasema hiyo ni idadi kubwa kabisa kwa mwaka kwa kipindi cha mungo mmoja uliopita.Hata hivyo safari hiyo pia ilighubikwa na vifo zaidi ya 90 na mwaka huu tayari watu 36 wamekufa maji katika tukio la Januari 8. Leo UNHCR imerejea onyo lake kwa watu wa Pembe ya Afrika wanaojaribu kuvuka bahari kuhusu hatari inayowakabili. Adrian Edwards ni msemaji wa UNHCR.

(SAUTI YA ADRIAN EDWARDS)

"Tukiangalia takwimu hizi kubwa na matatizo yanayoibuka kutokana na kuvuka bahari kote ulimwenguni, idadi hiyo inasikitisha. Watu wanazidi kuwasili licha ya hali ya kiusalama inayozidi kuzorota nchini Yemen, cha kusikitisha ni kwamba watu wengi wanazidi kupoteza maisha."

UNHCR Somalia na washirika wake wamekuwa wakishirikiana na jumuiya ya kimataifa na uongozi wa Somalia kuboresha hali ya kisiasa, usalama na , kiuchumi na kijamii nchini humo pamoja na kutafuta nsuluhu inayowezekana kwa wakimbizi, watu wanaorejea nyumbani na wakimbizi wa ndani.