Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR: Kamishina mkuu akaribisha vibali vya kufanya kazi kwa wakimbizi wa Syria

UNHCR: Kamishina mkuu akaribisha vibali vya kufanya kazi kwa wakimbizi wa Syria

Katika hatua ya mabadiliko makubwa ya sera, serikali ya Uturuki, imechapisha sheria mpya ambazo zinawaruhusu maelfu kati ya wakimbizi milioni 2.5 wa Syria waliopo nchini humo kuomba vibali vya kufanya kazi.

Wakimbizi walioorodheshwa na kuwemo Uturuki kwa takribani miezi sita wataruhusiwa kuomba vibali hivyo katika majimbo waliyowasili kwa mara ya kwanza .

Wasyria watakaokuwa na vibali vya kazi watalipwa angalau kiwango cha chini cha mshahara,. Hivi sasa kuna Wasyria wengi wanaofanya kazi kinyemela na wengi wao wanalipwa ujira mdogo sana. Akihojiwa na Redio ya Umoja wa Mataifa, msemaji wa UNHCR William Spindler amesema kupokea kiasi hicho cha wakimbizi ni mzigo mkubwa kwa Uturuki na hivyo Uturuki itahitaji kusaidiwa:

(Sauti ya Bwana Spindler)

Kuwepo kwa watu wengi kwenye nchi ni mzigo mkubwa kwenye kila eneo: afya, elimu, usafiri, huduma za maji, ajira, makazi, usalama na kadhalika… Uturuki inapaswa kuwa na uwezo wa kupokea idadi hiyo ya watu.  Muungano wa Ulaya hasa na nchi zingine pia zinapaswa kutafuta jinsi ya kuisadia Uturuki katika uamuzi huo wenye ujasiri.”

Kamishina Mkuu wa UNHCR Filipo Grandi amepongeza uamuzi huo na kusema ni wa kijasiri na hatua kubwa kwa mustakhbali wa wakimbizi. Hatua hiyo mpya itawagusa wakimbizi wote wanaoishi mijini na asilimia 10 walioko katika makambi ya wakimbizi.