Syria: maisha ya wakazi 200,000 wa Deir-ez-Zor iliyozingirwa hatarini

Syria: maisha ya wakazi 200,000 wa Deir-ez-Zor iliyozingirwa hatarini

Mashirika ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa yameelezea wasiwasi wao kuhusu watu wapatao 200,000, hasa wanawake na watoto, wanaozingirwa mkwenye mji wa Deir-Ez-Zor, nchini Syria.

Hayo yamesemwa na Stéphane Dujarric msemaji wa Umoja wa Mataifa akizungumza na waandishi wa habari leo mjini New York Marekani, akiongeza kwamba watu hawa wanahitaji misaada ya kibinadamu, hususan vyakula, vifaa vya kudhibiti utapiamlo na vifaa vya tiba, huku visa vya utapiamlo na unyafuzi vikiripotiwa.

Bwana Dujarric ameongeza kwamba akiba za chakula ni finyu sana mjini humo kwa sababu eneo halifikiki kutokana na mapigano. Hadi sasa ndege iliyokuwa ikibeba misaada haikuweza kutua kwa sababu ya mapigano yanayoendelea karibu ya uwanja wa ndege.

Wakati huo huo, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria, Staffan de Mistura amezungumza leo na wanachama wa Baraza la Usalama kwa njia ya video kuhusu maandalizi ya mazungumzo ya amani yanayotarajiwa kufanyika mjini Geneva.