Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi ya watalii duniani ilivunja rikodi mwaka 2015

Idadi ya watalii duniani ilivunja rikodi mwaka 2015

Idadi ya watu wanaosafiri nje ya nchi yao kwa ajili ya utalii iliongezeka kwa asilimia 4.4 mwaka 2015 na hivyo kuvunja rikodi mpya kwa mwaka wa sita mfululizo.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii UNWTO limesema kwenye taarifa yake kuwa idadi ya watalii ilifikia bilioni 1.2 mwaka 2015 na ongezeko hilo limechangia pakubwa katika ukuaji wa uchumi na uzalishaji wa ajira kwenye maeneo mengi ya dunia.

UNWTO imeongeza kwamba ni muhimu kwa serikali kukuza ukuaji wa sekta hiyo kupitia sera na uwekezaji.

Aidha imetarajia kuwa ongezeko hilo litaendelea mwaka 2016 hasa barani Asia na Pacifiki. Matarajio kwa Afrika na Mashariki ya Kati hayako thabiti kwa sababu ya vitisho vya usalama na ukosefu wa takwimu kamilifu.

Marekani, China na Uingereza ni nchi tatu zilizoshuhudia ongezeko kubwa la idadi ya watu waliosafiri kwenda nje ya nchi hizo kwa ajili ya utalii.