Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kitabu kipya cha FAO chapendekeza mbinu mpya za kilimo endelevu

Kitabu kipya cha FAO chapendekeza mbinu mpya za kilimo endelevu

Shirika la Chakula na Kilimo, FAO, limetoa leo kitabu kipya kinachopendekeza kubadili mfumo wa kuhifadhi na kuongeza mazao ya kilimo, kikitoa mwongozo wa kuweka mustakhabali endelevu kwa kilimo na kutimiza malengo ya maendeleo endelevu.

Kitabu hicho kinamulika jinsi uzalishaji wa nafaka kuu duniani, mathalan mahindi, mchele na ngano unavyoweza kufanywa kwa njia zinazoheshimu na kulinda mazingira.

Josef Kienzle ni mhandisi wa kilimo katika shirika la FAO

(Sauti ya Kienzle)

Tunachomaanisha hapa ni kilimo asilia, ambapo tunategemea uwezo wa mali asili na mchango wake kwa uzalishaji. Hiki kilisahauliwa zamani kidogo, ambapo tumeweka msisitizo kwa matumizi ya mbolea za kemikali na kilimo cha kutumia mashine, kwa kulima sana na kuharibu udongo. Kingine ni kupanda mimea aina ya kunde, ili kuongeza naitrojeni kwa njia asilia.”

Kitabu hicho kimekusanya mifano ya mifumo ya kilimo endelevu kutoka kote duniani ambayo tayari inatumiwa kwa ufanisi kuzalisha nafaka hizo zinazochangia asilimia 42.5 ya nguvu joto na asilimia 37 ya protini katika mwili wa mwanadamu.