Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua za dharura zahitajika kupunguza mateso gerezani Benin- UM

Hatua za dharura zahitajika kupunguza mateso gerezani Benin- UM

Kamati ya Umoja wa Mataifa kuhusu kuzuia utesaji, (SPT), imeitaka serikali ya Benin ichukue hatua mara moja ili kukabiliana na msongamano na mateso gerezani, na kuboresha hali ya ujumla ya walio vizuizini.

Kamati hiyo imesema hayo mwishoni mwa ziara ya wataalam wake nchini Benin, ambao wamesema kuwa ingawa Benin imepiga hatua kwa kiasi fulani tangu walipoitembelea mnamo mwaka 2008, bado kuna mengi ya kufanya.

Wataalam hao walioongonzwa na Bwana Victor Madrigal Borloz, wamesema kwamba wakati wa ziara yao ya hivi karibuni, vituo vingi vya kuzuilia mahabusu walivyotembelea vilikuwa na msongamano wa watu, na havikuwa na wahudumu wa kutosha na rasilmali nyingine.

Aidha, wameielezea serikali ya Benin kinagaubaga kuwa ili kuepusha mateso yaliyokithiri kwa wafungwa, ni muhimu kuboresha hima upatikanaji wa maji safi, chakula, kukabiliana na hali ya uchafu na kupunguza msongamano magerezani.