Skip to main content

UNAMID yatiwa hofu na mapigano huko Darfur ya Kati

UNAMID yatiwa hofu na mapigano huko Darfur ya Kati

Ujumbe wa pamoja wa Muungano wa Afrika na Umoja wa Mataifa huko Darfur, Sudan umesema una wasiwasi mkubwa kutokana na mapigano yanayoendelea huko Darfur Kati baina ya vikosi vya serikali na vikundi vilivyojihami.

Mapigano hayo ni kwenye eneo la Jebel Marra karibu na kituo cha UNAMID kilichoko Nertiti.

Katika taarifa yake UNAMID imeripoti kuangushwa kwa mabomu matano kwenye eneo karibu na kituo chake, ambako mtikisiko ulisikika na kusababisha hofu ya wakazi ambao walilazimika kufunga maduka yao kwa hofu ya kuporwa.

UNAMID imesema inafuatilia kwa karibu hali hiyo na inashirikiana na ofisi ya Umoja wa mataifa nchini humo na wadau wake juu ya hatua za kuchukua iwapo kuna athari kwa raia wa eneo hilo.

Kwa mara nyingine UNAMID imesisitiza umuhimu wa kufikia suluhu kwenye mzozo baina ya pande hizo kwa njia ya amani na kwamba iko tayari kusaidia.