Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tutapimwa kwa kuboresha maisha ya watu si kwa ahadi- Ban

Tutapimwa kwa kuboresha maisha ya watu si kwa ahadi- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amezungumza kwenye uzinduzi wa ripoti ya uchangiaji kwa masuala ya kibinadamu huko Dubai Falme za kiarabu na kusema kuwa wakati wa kusaka suluhu za muda mfupi kwa ajili ya misaada hiyo umekwisha.

Ban amesema hayo kwa kuzingatia kuwa majanga yanazidi duniani kila uchao na mahitaji yanaongezekwa kwani kwa mara ya kwanza katika Umoja wa Mataifa gharama za misaada ya kibinadamu zimezidi bajeti ya ulinzi wa amani.

(Sauti ya Ban)

 Hatua za usaidizi wa kibinadamu kwa sasa ndio zinagharimu zaidi Umoja wa Mataifa kuliko hata operesheni za ulinzi wa amani. Ripoti inaonyesha kuwa ilhali michango ya usaidizi wa kibinadamu inavunja rekodi, kiwango cha ukarimu nacho hakijawahi kufikia hali ya sasa ya kutotosheleza. Hatuwezi kuendelea namna hii. Tunahitaji fikra mpya na azma ya kufanya maamuzi magumu”

Ban amesema kinachoshuhudiwa sasa ni mgawanyiko kati ya misaada ya kibinadamu na ushirikiano wa kimaendeleo akinukuu ripoti iliyozinduliwa inayotaka ubia zaidi badala ya ushindani kati ya mashirika.

Kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu amesema ni vyema kuchukua hatua kwani tatizo la mmoja ni la mwingine kwa kuwa dunia sasa ni kijiji.

Amesema anaona suluhu katika hali hiyo kwa kuwa ni lazima kuchukua hatua kushughulikia majanga la sivyo changamoto zitaongezeka, pili hatua zitawezekana iwapo tu jamii ya kimataifa itapaza sauti moja na tatu mkutano ujao wa usaidizi wa kibinadamu ni fursa ya kuboresha duniani.

Ban amerejelea kauli yake aliyotoa mwaka 2006 wakati alipochaguliwa kuwa Katibu Mkuu, ya kwamba Umoja wa Mataifa hautapimwa kwa ahadi inazotoa bali kwa matokeo katika maisha ya watu wenye uhitaji zaidi.