Baraza la Usalama lalaani vikali shambulio la Ouagadougou

Baraza la Usalama lalaani vikali shambulio la Ouagadougou

Wajumbe wa baraza la usalama wamelaani vikali mashambulio ya kigaidi mjini Ouagadougou, Burkina Faso, yaliyotokea Ijumaa ya tarehe 15 Januari 2016, ambapo watu 29 wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa. Kundi la kigaidi la Al Mourabitoune, ambalo linauhusiano na kundi la Al-Qaida limekiri kuhusika na mashambulizi hayo.

Wajumbe wametuma salamu za rambirambi kwa familia za waathirika, serikali ya Burkina Faso, pamoja na kwa serikali ambazo raia wake wamelengwa katik a mashambulizi hayo. Pia wamewatakia nafuu ya haraka majeruhi.

Wajumbe hao wameelezea mshikamano wao na watu na uongozi wa Burkina Faso na nchi zingine katika ukanda mzima katika vita dhidi ya ugaidi na kusisitiza kwamba kuna haja ya kuongeza juhudi za kikanda na kimataifa kukabiloiana na ugaidi na ghasia zitokanazo na itikadi kali ambazo zinaweza kuwa chachu ya ugaidi.

Baraza la usalama limesisitiza kwamba ugaidi katika mifumo yote ni moja ya vitisho vikubwa zaidi kwa amani na usalama wa kimataifa.

Pia limesisitiza haja ya kuwafikisha wahusika wa ukatili huo katika mkono wa sheria, wakisema wote waliohusika na mauaji ni lazima wawajibishwe na kuyataka mataifa yote kutimiza wajibu wao chini ya sheria za kimataifa na maazimio ya baraza la usalama kwa kutoa ushirikiano ipasavyo katika suala hili.