Vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Iran vyaondolewa:IAEA

Vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Iran vyaondolewa:IAEA

Shirika la kimataifa la nishati ya atomiki, IAEA limetangaza kuondolewa kwa vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Iran kufuatia nchi hiyo kuanza kukidhi matakwa ya makubaliano ya mwezi Julai kati yake na mataifa yenye nguvu zaidi duniani.

Mkurugenzi Mkuu wa IAEA Yukia Amano ametangaza hatua hiyo leo , hatua ambayo imeungwa mkono pia na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon.

Bwana Amano amesema wakaguzi wa IAEA walithibitisha kuwa Iran imechukua hatua zote na hivyo inatoa fursa kwa IAEA kuanza kuthibtisha na kufuatiali azma ya Iran ya kutekeleza vipengele vya makubaliano hayo.

Miongoni mwa vipengele hivyo ni kutokomeza akiba ya Uranium iliyoboreshwa kwa kiwango cha kati na kupunguza kwa asilimia 98 Uranium iliyoboreshwa kwa kiwango kidogo.

Bwana Amano anasema..

"Uhusiano kati ya Iran na IAEA sasa unaingia awamu mpya. Ni muhimu kwa jamii ya kimataifa. Napongeza wote waliowezesha hatua hii kutokea. “

Iran ilitia saini makubaliano hayo tarehe 14 Julai 2015 huko Vienna, Austria na nchi Tano zenye ujumbe wa kudumu kwenye baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambazo ni China, Ufaransa, Urusi, Uingereza na Marekani. Ujerumani ambayo haina ujumbe wa kudumu nayo ilihusika kwenye makubaliano haya pamoja na Muungano wa Ulaya.