Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban na waziri wa Bahrain wajadili changamoto za usalama katika kanda

Ban na waziri wa Bahrain wajadili changamoto za usalama katika kanda

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon leo amezungumza kwa njia ya simu na waziri wa mambo ya nje wa ufalme wa Bahrain, Sheikh Khalid bin Ahmed Al Khalifa.

Miongoni mwa mambo waliyojadili ni hali katika eneo la Ghuba ya Uajemi ikiwa ni pamoja na changamoto za Amani na usalama katika kanda hiyo. Ban ameelezea matumaini yake kwamba nchi za ukanda huo zitachukua hatua madhubuti kupunguza mivutano iliyopo hivi sasa.

Ban pia amekubaliana na hatua zilizochukuliwa na serikali ya Bahrain kuboresha usalama na hali ya haki za binadamu. Amemchagiza waziri huyo na serikali kuchukua hatua zaidi za kukuza mazungumzo ya amani ya kisiasa miongoni mwa raia wote wa Bahrain na kuzingatia kikamilifu majukumu ya kimataifa ya haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha uhuru wa kujieleza, kukusanyika na uhuru mwingine wa msingi.

Mikakati hiyo si tu kukuza amani, usalama, maridhiano na ustawi katika Bahrain, lakini pia kuchangia kutatua mvutano katika kanda hiyo.