Skip to main content

Kisa kipya cha Ebola Sierra Leone, serikali na wadau wachukua hatua:WHO

Kisa kipya cha Ebola Sierra Leone, serikali na wadau wachukua hatua:WHO

Siku moja baada ya Shirika la afya duniani, WHO kutangaza kutokomezwa kwa Ebola huko Afrika Magharibi, mtu mmoja amefariki dunia kutokana na Ebola huko Sierra Leone na hivyo kutishia uwezekano wa kuibuka upya kwa kirusi hicho kwenye nchi hizo.

Msemaji wa WHO Geneva, Uswisi, Tarik Jasarevic amesema mgonwja huyo mwanamke alifariki dunia tarehe 12 mweiz huu na kwamba serikali ya Sierra Leone na wadau ikiwemo WHO wameshachukua hatua kupitia kituo cha operesheni za dharura dhidi ya Ebola. Hivyo amesema..

(Sauti ya Tarik)

“Hii kwa kweli inaaakisi kile tulichosema jana na katika taarifa zetu kwa umma kuwa bado kuna hatari na ugonjwa uko katika awamu muhimu kutoka kushughulikia wagonjwa na kwenda katika kuangalia hatari za mlipuko kama kifo hiki kilichoripotiwa. Ni muhimu watu waelewe siku 42 za ufuatiliaji zilizopita bila kisa siyo ishara ya kurejea nyumbani na kulegeza msimamo bali tuwe macho kudhibiti visa vipya.”

Sierra Leone bado iko katika kipindi cha siku 90 za ufuatiliaji wa uhakika dhidi ya Ebola tangu ugonjwa huo utangazwe kutokomezwa nchin humo tarehe 07 Novemba 2015.

Lengo la kipindi hicho ni kuhakikisha hakuna mlolongo wowote wa maambukizi uliofichika na iwapo kuna mlipuko wowote uweze kudhibitiwa.