Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zeid aonya kuibuka kwa ukiukwaji mpya wa haki Burundi ikiwemo unyanyasaji wa kijinsia:

Zeid aonya kuibuka kwa ukiukwaji mpya wa haki Burundi ikiwemo unyanyasaji wa kijinsia:

Tunaanzia Burundi, Kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa mataida  Zeid Ra’ad Al Hussein ametoa taarifa akiionya Burundi juu ya kuibuka kwa mwenendo mpya unaotia wasiwasi ikiwa ni pamoja na kesi za unyanyasaji wa kijinsia unaofanywa na vikosi vya usalama na ongezeko kubwa la kupotea kwa watu na visa vya mateso. Flora Nducha na taarifa kamili..

(TAARIFA YA FLORA NDUCHA)

Kwa mujibu wa Zeid wameorothesha visa 13 vya unyanyasaji wa kijinsia vilivyoanza wakati wa operesheni za kusaka na kukamata watu baada ya matukio ya Desemba , na visa vingine vimeendelea ikiwemo taarifa za ubakaji wa wanawake watano kwenye nyumba moja jimbo la Maire mjini Bujumbura.

Pia ametoa wito wa kufanyika uchunguzi wa haraka dhidi ya vitendo vilivyotokea tarehe 11 na 12 Desemba mjini Bujumbura zikiwemo taarifa za kuwepo kwa makaburi tisa ya pamoja. Rupert Colville ni msemaji wa ofisi ya haki za binadamu.

(SAUTI YA RUPERT COLVILLE)

“Kwa sasa tunachambua  picha za setelaiti ili kupata uelewa zaidi wa tuhuma hizi nzito, na kama alivyosema kamishna mkuu katika taarifa yake,   ishara zote zinadhihirisha tahadhari ya hali ya juu kabisa ikiwemo kupanuka kwa wigo wa janga la kikabila.”