Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa WFP yuko ziarani Zambia

Mkuu wa WFP yuko ziarani Zambia

Mkurugenzi mtendaji wa shirika la mpango wa chakula duniani WFP Ertharin Cousin, anafanya ziara ya kikazi nchini Zambia. Amewasili leo Alhamisi mjini Lusaka na atakuwepo nchini humo hadi Januari 17.

Ziara yake imekuja wakati ambapo ukame na msimu wa eli Nino umeathiri pakubwa Kusini mwa Afrika hususani wakulima wadogowadogoambao ndio wazalishaji wakubwa katika eneo hilo.

Zambia ina jukumu kubwa katika ukanda huu ikizingatiwa kuwa  ndio mzalishaji na msafirishaji mkubwa wa mahidi na mazao. Wakati wa ziara yake atakutana na Rais  Edgar Lungu, makamu wa Rais  Inonge Wina, wawakilishi kutoka wizara mbalimbali, na jamii ya wafanyabiashara na wadau wa maendeleo.

Atajadili na viongozi hao miradi mbalimbali ikiwemo msaada wa WFP wa kuchagiza mpango wa mlo mashuleni ambapo serikali inachangia pakubwa mwaka huu. Pia atatembelea miradi miwili ya WFP iliyopo jimbo la Kusini mwa nchi hiyo inayowasaidia wakulima wadogowadogo.