Wasiwasi waongezeka nchini DRC: MONUSCO
Uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ni changamoto kubwa ya mwaka 2016, amesema leo Maman Sidikou, Mwakalishi Maalum wa Katibu Mkuu nchini humo, akihutubia Baraza la Usalama. Taarifa zaidi na Flora Nducha.
(Taarifa ya Flora)
Akiripoti kwa njia ya video kutoka mji mkuu wa DRC, Kinshasa, Bwana Sidikou amesema uchaguzi huo umeshaanza kusababisha mivutano, huku visa 260 vya ukiukwaji wa haki za binadamu vikiwa vimeripotiwa tangu mwaka uliopita, akiongeza.
(Sauti ya Bwana Sidikou)
“Bila makubaliano kuhusu mchakato wa uchaguzi, mganwanyiko wa kisiasa umeeneza mivutano na kuchangia katika mazingira ya unyanyapaa na ukiukwaji wa haki za binadamu. Hii inaonyesha mwelekeo unaotia wasiwasi kuhushu kubinywa kwa fursa za kushiriki kwenye maswala ya kisiasa na ni changamoto katika kutekeleza kwa amani uchaguzi unaoaminika.”
Kuhusu hali ya kiusalama, amesema hali imezorota sana Mashariki mwa nchi kwa kipindi cha wiki chache zilizopita licha ya jitihada za jeshi la kitaifa na vikosi vya MONUSCO.
Hata hivyo ameeleza kwamba MONUSCO itapunguza askari wake 1,700 bila kudhoofisha nguvu zake za kupambana na waasi.