Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwaka 2016 wapaswa kuwa mwaka wa utekelezaji: Ban

Mwaka 2016 wapaswa kuwa mwaka wa utekelezaji: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon leo amehutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwenye makao makuu New York, Marekani na kutangaza malengo yake kwa mwaka huu wa 2016.

Katika hotuba yake ametaja mafanikio yaliyopatikana mwaka 2015, yakiwemo makubaliano kuhusu tabianchi, ajenda ya maendeleo ya 2030, makubaliano ya kisiasa kuhusu Iran, huku akitaka kuwekea utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu SDGs akisema:

“ Kila serikali inapaswa kuonyesha kwamba inamiliki malengo hayo kwa kuandaa sera, sheria na ufadhili kwa ajili ya malengo ya maendeleo endelevu.”

Ameorodhesha pia ugaidi, madawa ya kulevya, ukimbizi, na ajira kwa vijana miongoni mwa maudhui yatakoyaangaziwa mwaka huu.

Aidha amezingatia amani kama msingi wa kupata maendeleo duniani akimulika umuhimu wa kushughulikia mizizi yake ikiwemo ugaidi na ukiukaji wa haki za binadamu.

Hatimaye amekariri msimamo wa Umoja wa Mataifa kuhudumia watu wote duniani, hasa wanaoteseka zaidi akitumai kwamba mwaka 2016 utakuwa mwaka wa kuchukua hatua thabiti.