Maambukizi ya Ebola Liberia yameisha, nchi zote 3 sasa huru- WHO
Shirika la Afya Duniani, WHO limetangaza kuwa Liberia sasa imeondolewa kwenye orodha ya nchi ambako maambukizi ya kirusi cha Ebola yanaendelea.
Tangazo hili linakuja siku moja baada ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kufanya kikao kuhusu Ebola, ambapo Katibu Mkuu Ban Ki-moon alipongeza juhudi za jamii ya kimataifa katika kupambana na homa hiyo.
Kuhusu hatua hii ya ufanisi, Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dr. Margaret Chan amesema
(Sauti ya Dkt. Chan)
“Hii ni mara ya kwanza kabisa kwa nchi zote tatu kuripoti visa sifuri kwa angalau siku 42, ambazo ni mara mbili ya kipindi cha kusubiria kuona kama kuna maambukizi mapya. Huu, mabibi na mabwana, ni ufanisi mkubwa mno”
Tangu ilipolipuka mnamo Disemba mwaka 2013, homa ya Ebola imewaua watu zaidi ya 11,300, hususan katika nchi za Liberia, Sierra Leone, na Guinea ambako iliripotiwa kwanza.
Sierra Leone ndiyo iliyokuwa ya kwanza kutangaza kumalizika kwa maambukizi ya Ebola mnamo Novemba 7 mwaka 2015, ikifuatiwa na Guinea mnamo Disemba 29, 2015.