Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ebola ilitoa mtihani mkubwa kwa nguvu na utashi wetu; tusilegee - Ban

Ebola ilitoa mtihani mkubwa kwa nguvu na utashi wetu; tusilegee - Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, amesema leo kuwa kuibuka kwa mlipuko wa homa ya Ebola katika nchi za Afrika Magharibi, ulikuwa mtihani mkubwa kwa nguvu na utashi wa pamoja, lakini jamii ya kimataifa iliongeza nguvu jitihada zake, na leo hii hali ni tofauti sana.

Ban amesema hayo akilihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, wakati likikutana kupokea ripoti kuhusu Ebola, siku moja kabla ya kutangazwa kukomeshwa kwa maambukizi nchini Liberia na katika eneo zima.

Ban amesema ingawa ufanisi mkubwa umefikiwa kufikia sasa, changamoto bado zipo, zikiwemo uwezekano wa kuibuka maambukizi mapya siku zijazo, na kwamba kuna mengi ya kujifunza, na kazi nyingi ya kufanya.

“Kumalizika kwa maambukizi ya Ebola Afrika Magharibi ni ushahidi wa ufanisi tunaoweza kufikia ushirikiano unapofanya kazi ipasavyo, kwa kuleta pamoja nguvu za jamii ya kimataifa na serikali za kitaifa katika kuwahudumia watu. Tutoe ahadi ya kuendeleza umakinifu wetu na mshikamano wetu kwa watu wa Afrika Magharibi na ulimwengu wetu.”

Akiongea kutoka Geneva kwa njia ya video, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, WHO, Dr. Margaret Chan, amesema

“Tumepiga hatua kubwa katika kushinda mlipuko mkubwa zaidi na tatanishi zaidi wa Ebola katika historia. Kileleni mwa mlipuko wa Ebola miezi 15 iliyopita, zaidi ya visa 900 vipya vya Ebola vilikuwa vikiripotiwa kila wiki. Sasa zimepita wiki sita bila kisa chochote. Kesho, Januari 14, Liberia itaondolewa kwenye orodha ya nchi kunakoendelea maambukizi ya Ebola”