Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kongamano lafanyika kuendeleza haki za binadamu katika nchi za Kiarabu

Kongamano lafanyika kuendeleza haki za binadamu katika nchi za Kiarabu

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa, Zeid Ra’ad Al Hussein, ametoa wito kwa nchi za Kiarabu zijiunge hima kwa mikataba yote ya msingi kuhusu haki za binadamu, na kuhakikisha kuwa inafuatwa na kutekelezwa.

Kamishna Zeid amesema hayo akishiriki katika kongamano la siku mbili kuhusu mchango wa Ofisi yake katika kuendeleza na kulinda haki za binadamu katika eneo la nchi za Kiarabu mjini Doha, Qatar.

Kamisha Zeid ameongeza kuwa, ingawa nchi za Kiarabu zimepiga hatua kubwa katika kuridhia maagano na mikataba ya haki za binadamu, pamoja na sheria ya kimataifa ya kibinadamu, hali halisi inaonyesha kuwa raia wao hawajanufaika katika maisha yao kutokana na hatua hizo, kwani hapajawa na utekelezaji upasao wa mikataba hiyo.

Amesema kanuni za sheria ya kimataifa ya kibinadamu kuhusu ulinzi wa raia, watoto, wanawake na wazee, sehemu za ibada na hospitali, zote zimejumuishwa katika mafunzo ya dini ya Kiislamu.

Kongamano hilo la Januari 13 na 14 linazileta pamoja nchi za eneo la Kiarabu, mashirika yasiyo ya kiserikali, watetezi wa haki za binadamu na watu wanaojali haki za binadamu.