Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msaada wa wahisani waisaidia WFP kundelea na huduma za ndege Sudan

Msaada wa wahisani waisaidia WFP kundelea na huduma za ndege Sudan

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP limekaribisha mchango mkubwa kutoka kwa wahisani uliosaidia operesheni zake za huduma za ndege za kibinadamu za Umoja wa Mataifa (UNHAS) nchini Sudan kwa mwaka 2015.

Shirika hilo limesema michango hiyo iliyofika kwa wakati kutoka fuko la fedha la kibinadamu CHF, tume ya Ulaya ya misaada ya kibinadamu na idara ya ulinzi kwa raia ECHO, na serikali za Uingereza, Sweden na Switzerland kuhakikisha kwamba WFP, ambayo inasimamia UNHAS inaendelea kutoa huduma muhimu kwa wafanyyakazi wa misaada nchini Sudan hadi mwisho wa mwaka 2015.

UNHAS inafadhiliwa na michango ya wahisani mbali ya gharama ndogo inayolipwa na abiria. Mwaka 2015 UNHAS pia ilipata msaada wa fedha kutoka kwa serikali za Marekani, Ujerumani na Canada.

Huduma ya UNHAS ilianzishwa nchini Sudan mwaka 2004 kutoa huduma ya usafiri unaoaminika kwa mizigo na abiria ambao ni wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu nchini humo. Hivi sasa inatoa huduma kwa mashirika 100 yakiwemo ya Umoja wa mataifa na wadau wa misaada ya kibinadamu.