Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mazungumzo ya de Mistura na P5 Geneva kuhusu Syria yaweka nuru

Mazungumzo ya de Mistura na P5 Geneva kuhusu Syria yaweka nuru

Mkutano kati ya mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria, Staffan de Mistura, na wawakilishi wa nchi tano zenye ujumbe wa  kudumu wa baraza la usalama P5, ni fursa ya kuwapatia taarifa za karibuni zaidi baada ya ziara  yake kwenye ukanda husika.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa Bwana de Mistura aliitisha kikao hicho kufuatia ziara yake huko Mashariki ya Kati ambapo imeleta matokeo ya mwonekano wa maandalizi ya mazungumzo ya Geneva kuhusu Syria.

Katika kuelekea mazungumzo ya Syria tarehe 25 mwezi huu, Bwana de Mistura ametumia kikao cha leo kusaka utambuzi wa nchi hizo tano katika kubaini umuhimu wa wananchi wa Syria kufikiwa na huduma bila vikwazo vyovyote hata kwenye maeneo yaliyozingirwa .

Maafisa wa nchi hizo Tano wamekubali kushinikiza hatua za haraka za kusaidia jitihada hizo katika siku chache zijazo.

Taarifa hiyo imesema bwana de Mistura na ujumbe wake wataendelea na suala la mialiko ili kuhakikisha mazungumzo kuhusu Syria yanakuwa shirikishi na jumuishi kwa minajili ya kuona yanafanyika Geneva kama ilivyopangwa.