Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mindaoudou aliambia Baraza la Usalama Cote d’Ivoire bado inakabiliwa na changamoto nyingi

Mindaoudou aliambia Baraza la Usalama Cote d’Ivoire bado inakabiliwa na changamoto nyingi

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limefanya kikao leo kuhusu hali nchini Cote d’Ivoire, ambapo Mwakilishi wa Katibu Mkuu nchini humo, Aïchatou Mindaoudou, ameliambia Baraza hilo kuwa nchi hiyo bado inakabiliwa na changamoto nyingi, licha ya ufanisi katika uchaguzi wa rais na kuboreka kwa hali ya usalama. Taarifa kamili na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Akitaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana nchini Cote d’Ivoire, Bi Mindaoudou amesema kuhakikisha usalama wakati wa uchaguzi mwezi Oktoba mwaka uliopita ulikuwa mtihani mkubwa, na kwamba licha ya dosari kidogo, vikosi vya usalama viliweza kuzishinda changamoto hizo.

Ameongeza kuwa ingawa bado kuna changamoto ya ujangili na ugaidi, uhalifu wa kikatili pia umepungua, na kwamba juhudi nyingi zimeelekezwa katika kukabiliana na ukatili wa kingono. Licha ya hayo, Bi Mindaoudou amesema bado nchi hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi, akitaja mambo yanayopaswa kufanywa..

(Sauti ya Mindaoudou)

“Bado changamoto zipo, zikiwa ni kuendeleza mchakato wa maridhiano ya kitaifa, kuboresha sekta ya usalama, hasa mabadiliko   kwenye jeshi na polisi, kurejesha askari wa zamani kwenye maisha ya kawaida, pamoja na kuimarisha hali ya haki za binadamu, na sheria ya mpito. Ni changamoto za msingi kwa Cote d’Ivoire inapokuwa kwenye njia ya kufikia utulivu wa kudumu.”