Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sekta ya ndege na meli zitozwe kodi za utoaji hewa ya ukaa:IMF

Sekta ya ndege na meli zitozwe kodi za utoaji hewa ya ukaa:IMF

Shirika la fedha duniani, IMF limependekeza sekta ya usafiri wa anga na majini kuwekewa kodi ya utoaji wa hewa ya ukaa kama njia mojawapo ya kufikia malengo ya kimataifa ya kudhibiti mabadiliko ya tabianchi.

Katika ripoti yake, IMF imekadiria kuwa iwapo dola 30 itatozwa kwa kila tani moja yah hewa ukaa kwenye sekta hizo itachangia dola bilioni 25 ambazo zitasaidia nchi zinazoendelea kuimarisha mipango yao ya kuhimili na kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi.

IMF inasema hewa chafuzi ya ukaa kutoka kwenye ndege na meli inasababisha karibu asilimia nne katika kiwango cha hewa ukaa duniani na suala hilo halikuguswa moja kwa moja wakati wa mjadala wa mkataba mpya wa mabadiliko ya tabianchi uliopitishwa Paris, Ufaransa mwishoni mwa mwaka jana.

Ripoti hiyo imesema mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayohusika na usafiri wa anga na majini yatawajibika kuweka kanuni za utekelezaji wa mpango huo.

IMF imesema inatambua kuwa na changamoto katika kuanzisha kodi hiyo lakini changamoto hizo zinaweza kukabiliwa.