Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama latoa wito kuhusu mchakato wa amani Mali

Baraza la Usalama latoa wito kuhusu mchakato wa amani Mali

Wanachama wa Baraza la Usalama wamekaribisha hatua za awali zilizochukuliwa na serikali ya Mali katika utekelezaji wa makubaliano ya amani wakiisihi kuchukua harakati zinazotakiwa ili kuendeleza utaratibu wa amani pamoja na vyama vya upinzani na vikundi vilivyojihami.

Miongoni mwa hatua zinazohitajika ni kuandaa doria za usalama za pamoja kaskazini mwa nchi, kutekeleza mpango wa kusalimisha waasi na kuanzisha mchakato wa kupeleka madaraka kwenye serikali za mitaa.

Taarifa iliyotolewa jumanne na Baraza la Usalama imekariri mshikamano wake na mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini humo aliyeteuliwa hivi karibuni, Mahamat Saleh Annadif, ikiziomba pande kinzani kushirikiana naye katika utekelezaji wa majukumu yake.

Aidha wanachama wa Baraza hilo wameelezea wasiwasi wao kuhusu hali ya usalama nchini humo, ikiwemo kuenea kwa vitisho vya kigaidi, wakiziomba nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zinazochangia katika kupeleka askari kwenye Ujumbe wa Umoja huo nchini Mali, MINUSMA kuhakikisha vikosi hivyo vina vifaa na mafunzo ya kutosha.