Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uenyekiti wa G-77 na China; Afrika ya Kusini yakabidhi kijiti kwa Thailand

Uenyekiti wa G-77 na China; Afrika ya Kusini yakabidhi kijiti kwa Thailand

Matukio na maamuzi mengi ya kihistoria yaliyopitishwa mwaka 2015 hayangalikuwa na mafanikio bila ya ushirika thabiti wa kundi la nchi 77 na China.

Ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon aliyotoa jijini New York, Marekani wakati wa makabidhiano ya uenyekiti wa kundi hilo kwa Thailand baada ya Afrika Kusini kuhitimisha muda wake wa uongozi wa mwaka mmoja.

Ban amesema malengo ya maendeleo endelevu au ajenda 2030 ni miongoni mwa hatua thabiti za mwaka 2015 ambazo amesema zinaweka mwelekeo wa dunia katika miaka 15 ijayo.

Ametaja pia mkataba wa mabadiliko ya tabianchi nchi uliopitishwa Paris, Ufaransa akisema ni kiashiria cha ushindi wa ushirikiano wa kimataifa.

Amesema sasa jukumu limesalia katika utekelezaji hivyo ni matumaini yake kuwa kundi la nchi 77 na China litaendelea na usukani akilisihi kundi hilo chini ya uongozi wa Thailand iwe mstari wa mbele kwenye tathmini ya mwaka huu ya sera za Umoja wa Mataifa.

Tathmini hiyo hufanyika kila baada ya miaka minne.

Katibu Mkuu amesema Umoja wa Mataifa kwa upande wake utakuwa pamoja na kundi hilo.