Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa kusomesha watoto wakimbizi wa Syria wapata milioni 250

Mradi wa kusomesha watoto wakimbizi wa Syria wapata milioni 250

Mradi wa dharura wenye lengo la kusaidia watoto wakimbizi wa Syria milioni moja kurejea shuleni umepata ufadhili wa dola milioni 250, amesema leo Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu kwa Wote, Gordon Brown.

Ameeleza kwamba ufadhili huo wa kwanza umeahidiwa na Muungano wa Ulaya na sekta ya kiserikali na binafsi kutoka nchi za Uarabuni.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York Marekani kwa njia ya video kutoka Uingereza, Bwana Brown amemulika janga la watoto wa Syria wanaoishi ukimbizini na kutumikshwa au kuozeshwa bado wadogo.

Bwana Brown amesema bado dola milioni 500 zinahitajika ili kutekeleza mradi huo nchini Lebanon, Uturuki na Jordan. Amesema tayari mradi wa jaribio uliotekelezwa Lebanon umeonyesha nuru watoto 207,000 wakiwa wanasoma kwa zamu mbili kwa siku nchini humo.

(Sauti ya Bwana Brown)

“ Safari za kifo za kwenda Ulaya hazitapungua bali kuongezeka sana mwaka 2016 iwapo watoto wa Syria milioni sita ambao ni wakimbizi wa ndani na milioni mbili ambao ni wakimbizi bado wanatumikishwa na kunyimwa fursa yoyote kwenye ukanda huo.”

Ameongeza kwamba lengo ni kuhakikisha watoto wote milioni 30 wanaoishi ukimbizini wanapewa fursa ya kusoma ifikapo mwaka 2017.