Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IOM yasaidia baada ya meli kuzama pwani ya Somaliland

IOM yasaidia baada ya meli kuzama pwani ya Somaliland

Wahamiaji 36 wamekufa maji wakati meli iliyokuwa imebeba wahamiaji 106 , wasomali na Waethiopia  kuzama pwani ya jimbo lililojitenga la Somaliland kaskazini mwa Somalia siku ya Ijumaa, limesema shirika la kimataifa la uhamiaji IOM.

IOM, ikishirikiana na kitengo cha usaidizi kwa wahamiaji Somaliland (MRC) wanausaidia uongozi wa Somaliland kwa kugawa chakula, maji na madawa kwa manusura. Pia wanatoa malori kwa ajili ya kuwahamisha wahamiaji hao kutoka Harasho walikozama hadi miji ya Sanaag na Erigavo ili kupata matibabu.

Kwa mujibu wa MRC , manusura wote walikuwa na upungufu wa maji mwilini na wamedhoofu huku wengi wao wakihitaji huduma ya afya ya dharura na waliokuwa mahututi walikimbizwa kwenye hospitali za katribu ambako wamekuwa wakipewa matibabu na timu ya waunguzi ya IOM.

Wahamiaji hao wakiwa katika afueni ya kuweza kusafiri IOM kwa kushirikiana na shirika la kuhudumia wakimbizi UNHCR, na wadau wengine wa serikali watawahamishia kwenye kituo cha Berbera kinachosimamiwa na UNHCR ambako watalala, kuandikishwa  na kufanyiwa tathimini ya mahitaji yao.

Wasomali, Waeritrea na Waethiopia ndio idadi kuwa ya wahamiaji wanaojaribu kuvuka Ghuba ya Aden na bahari ya Sham wakijaribu kuingia Yemen na kwingineko wakitumia usafiri hatari wa boti.