Nyumba 1,000 za wakimbizi zateketezwa kwa moto Sudan Kusini
Kambi ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS inayowapa hifadhi raia 48,000 tangu Disemba 2013 kwenye eneo la Malakal imeteketezwa kwa moto, amesema leo msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric akizungumza na waandishi wa habari mjini New York, Marekani.
Bwana Dujarric amesema moto huo ambao ulianza jumapili umeshadhibitiwa baada ya kusababisha pia kifo cha mtoto mmoja, watu nane kujeruhiwa na nyumba 1,000 kuteketea. Hadi sasa chanzo cha moto hakijajulikana.
Wakati huo huo, Bwana Dujarric amesema UNMISS imeripoti vifo vya askari watatu wa jeshi la kitaifa SPLA na raia watatu baada ya lori walimokuwa wakisafiria kulipuliliwa na gruneti kwenye eneo la Malakal. Watu 12 wamejeruhiwa katika mlipuko huo na wamepelekwa kwenye hospitali ya UNMISS.