Skip to main content

Miaka 6 baada ya tetemeko la ardhi Haiti, changamoto bado nyingi

Miaka 6 baada ya tetemeko la ardhi Haiti, changamoto bado nyingi

Kuelekea miaka sita tangu kutokea kwa tetemeko kubwa la ardhi lililoua zaidi ya watu 200,000 nchini Haiti tarehe 12, Januari, 2010, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameeleza mshikamano wake na familia za wahanga.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York Marekani, msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric amemnukuu Katibu Mkuu akitoa wito kwa jamii ya kimataifa kuendelea kusaidia Haiti katika jitihada za kujenga nchi upya, akiongeza kwamba kupata nafuu tena siyo rahisi, raia wengi wa Haiti wakiendelea kukumbwa na changamoto nyingi.

Bwana Dujarric ameeleza kwamba Haiti inaendelea kuhitaji misaada, watu wengi wakiwa bado ni wakimbizi wa ndani, wengine wakikumbwa na ukosefu wa chakula au huduma za maji na kujisafi.

Aidha amesema kwamba Katibu Mkuu ametoa heshima kwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa 102 waliopoteza maisha kwenye tukio hilo, akikariri msimamo wa Umoja wa Mataifa kuendelea kusaidia Haiti katika kutimiza dira yake kwa mustakabali wenye maendeleo na demokrasia.