Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wanaokimbia Yemen bila walezi watafuta usalama Somaliland

Watoto wanaokimbia Yemen bila walezi watafuta usalama Somaliland

Zaidi ya watoto 9,500 kutoka Yemen wamekimbia machafuko nchini humo na kutafuta usalama katika jimbo huru la Somaliland nchini Somalia, wakiwa peke yao bila wazazi au walezi, kwa mujibu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi katika Umoja wa Mataifa, UNHCR.

UNHCR imesema watoto hao ni miongoni mwa zaidi ya watoto 168,000 ambao wamekimbia machafuko nchini Yemen tangu Machi mwaka huu, kufuatia kuibuka kwa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, baada ya miaka mingi ya misukosuko ya kisiasa na kiuchumi, na mivutano ya kidini.

Wengi wa watoto hao ni wa raia wa Ethiopia na Somalia, ambao zamani walikimbilia Yemen wakitafuta usalama, ingawa miongoni mwao kuna zaidi ya watoto 2,600 wenye asili ya Yemen, wakiwemo 850 waliojiandikisha na UNHCR wakiwa hawana jamaa zao wa karibu.