Skip to main content

Sudan Kusini yaongoza kwa kuwa na watoto wasiokwenda shule:UNICEF

Sudan Kusini yaongoza kwa kuwa na watoto wasiokwenda shule:UNICEF

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema watoto takribani Milioni 24 walio katika nchi 22 zenye mizozo hawako shuleni.

Katika taarifa yake ya leo, UNICEF imesema Sudan Kusini ndiyo yenye idadi kubwa zaidi ambako zaidi ya nusu ya watoto wenye umri wa kuwa shule za msingi na sekondari hawako shuleni. Nchi ya pili ni Niger, ikifuatiwa na Sudan na Afghanistan.

Akihojiwa na redio ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva Uswisi, msemaji wa UNICEF Christophe Boulierac amesisitiza umuhimu wa kutoa huduma za elimu wakati wa mizozo.

(Sauti ya Bwana Boulierac)

"Elimu ni ulinzi kwa watoto kwenye mizozo. Na wakienda shuleni, hatari ya kukumbwa na ukiukwaji inapungua. Kwa kipindi cha muda mrefu watoto wasipoenda shuleni, na kizazi kizima kikiwa hakiwezi kwenda shuleni, inatishia maendeleo na afya ya nchi nzima."