Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtandao wa kukodisha baiskeli New York wafikia Milioni 10 mwaka jana

Mtandao wa kukodisha baiskeli New York wafikia Milioni 10 mwaka jana

Mpango wa utekelezaji wa hatua kuhusu mabadiliko ya tabianchi, ClimateAction unaofanya kazi kwa ubia na shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP umezungumzia mafanikio ya mtandao wa kukodisha baiskeli kwenye jiji la New York, nchini Marekani.

Mtandao huo umemnukuu Meya wa New York, Bill de Blasio akisema kuwa kwa mwaka jana pekee mtandao huo umehudumia watu Milioni 10 kutokana na baiskeli 7,500 zinazokodishwa kwenye jiji hilo, ambapo matumizi hayo ni ongezeko kwa asilimia 24.

Mpango ni kuongeza baiskeli hadi zifikie 12,000 mwakani ambapo ofisi ya Meya imesema mtandao huo sasa unakwenda sambamba na mfumo wa kukodisha baiskeli kwa nchi za magharibi.

Utafiti  unaonyesha kuwa mpango huo ulioanzishwa mwaka 2013, umewezesha kupunguza msongamano wa magari na kuzuia magari mengi kuingia jijini New York na hivyo kupunguza uchafuzi wa mazingira sanjari na kuwezesha watumaiji kufanya mazoezi.