Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban alaani shambulio dhidi ya hospitali huko Yemen

Ban alaani shambulio dhidi ya hospitali huko Yemen

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelaani shambulio dhidi ya hospitali inayoendeshwa na madaktari wasio na mipaka, MSF huko jimbo la Sa’ada nchini Yemen ambalo limesababisha vifo vya watu wanne.

Mpaka sasa bado haijafahamika ni nani aliyefanya shambulio hilo la Jumapili ambalo pia limesababisha majeruhi kadhaa.

Ban kupitia taarifa ya msemaji wake ametuma rambi rambi kwa familia za wafiwa na wananchi wa Yemen kufuatia shambulio hilo ambalo ni miongoni mwa mashambulio dhidi ya vituo vya afya nchini humo kufuatia yale ya mwaka 2015.

Katibu Mkuu amesema ana hofu kubwa juu ya kuongezeka kwa mkwamo wa kufikia vituo vya afya akisisitiza kuwa hospitali na wahudumu wa afya wanalindwa na sheria za kimataifa za kibinadamu.

Amesema shambulio lolote la makusudi dhidi yao au miundombinu yoyote ya kiraia ni ukiukwaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu.

Ban ametaka uchunguzi huru na wa haraka ufanyike dhidi ya shambulio hilo akirejelea wito wake kwa pande husika kwenye mzozo wa Yemen kusitisha chuki baina  yao na badala yake kusaka suluhu la amani kupitia mashauriano  yanayoongozwa na mjumbe wake.