Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM watoa dola milioni 7 kwa misaada ya kibinadamu eneo la Ziwa Chad

UM watoa dola milioni 7 kwa misaada ya kibinadamu eneo la Ziwa Chad

Mratibu wa masuala ya kibinadamu katika Umoja wa Mataifa,  Stephen O’Brien, ameidhinisha utoaji wa dola milioni saba za Kimarekani kutoka mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Misaada ya Dharura, CERF, kwa minajili ya kutoa usaidizi wa kibinadamu katika eneo la Ziwa Chad.

Kuendelea kwa machafuko na athari za kiuchumi na kijamii kutokana na hali mbaya ya usalama katika eneo hilo, zimelazimu zaidi ya raia 50,000 wa Chad kukimbia visiwa vya Ziwa Chad kati ya Julai na Disemba 2015 na kutafuta hifadhi katika kambi za wakimbizi wa ndani, vijijini na katika wilaya mbali mbali.

Halikadhalika, kuna wakimbizi 15,000 wa Chad waliorejea kutoka Nigeria, wakimbizi wa Nigeria 14,000 na wakimbizi wengine 700 kutoka nchi zingine, wanaohitaji usaidizi wa kibinadamu. Hali hiyo ya wakimbizi pia imeathiri jamii za wenyeji, ambazo miongoni mwao, watu 112,000 wanahitaji msaada.