Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Huduma za afya kwa wazee Afrika Mashariki

Huduma za afya kwa wazee Afrika Mashariki

Uzee hutizamwa na jamii kama kipindi kigumu kilichojawa na kadhia nyingi. Moja ya kadhia inayokumba kundi hili ni  upatikanaji wa huduma za kijamii mathalani afya.

Malengo mapya ya maendeleo endelevu SDGS yaliyoridhiwa na nchi wanachama hivi karibuni yanaanisha nafasi ya wazee katika kupatiwa huduma ya afya na kuangalia ustawi wao kwa ujumla. Lengo namba tatu lisemalo afya bora na ustawi pamoja na makundi mengine katika jamii linaangazia afya za wazee ambao mara nyingi husahaulika.

Akisisitiza umuhimu wa kujumishwa kwa kundi hilo wakati wa siku ya kimataifa ya wazee, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema  kuna haja ya kuandaa miji jumuishi na mujarabu kwa ajili ya wazee ikimaanisha kukuza fursa za kiuchumi na ushirikishwaji wa kijamii na mazingira salama.

Ban amekwenda mbali zaidi na kusema kuwa utolewaji wa nyumba rahisi na afya  pamoja na huduma za kijamii ambazo zinahitajika wakati wa uzee ni moja ya maisingi muhimu katika jamii.