Skip to main content

Ban ahofia mashambulizi ya anga na mapigano Yemen

Ban ahofia mashambulizi ya anga na mapigano Yemen

Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon amesema anatiwa hofu na ongezeko la mashambulizi ya pamoja ya anga , mapigano ya ardhini na uvurumishaji wa makombora nchini Yemen, licha ya wito uliotolewa mara kadhaa wa kusitisha mapigano.

Ban amesema hofu yake kubwa ni hususan mashambuzi ya anga kwenye maeneo ya amakazi ya watu na majengo ya raia mjini Sana’aikiwemo jengo la chama cha wafanyabiashara, ukumbi wa sherehe za harusi na kwenye kituo cha watu wasioona.

Pia amepokea taarifa za kusikitisha za matumizi ya mambomu mtawanyiko katika mashambulizi yaliyofanyika Sana’a Januari 6 katika maeneo mbalimbali.

Ameongeza kuwa matumizi ya mambomu mtawanyiko kwenye makazi ya watu inaweza kuwa ni uhalifu wa kivita kutokana na uuaji wake wa kiholela.

Ban amezikumbusha pande zote kuheshimu wajibu wao chini ya sheria za kimataifa za haki za binadamu ambazo zinakataza mashambulizi ya kulenga dhidi ya raia na miundombinu ya raia.