Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM wakaribisha kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi CAR

UM wakaribisha kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi CAR

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR Parfait Onanga-Anyanga amekaribisha tangazo la matokeo ya Uchaguzi wa rais na wabunge yaliyotangazwa leo nchini humo.

Taarifa iliyotolewa leo na idara ya operesheni za kulinda amani ya Umoja wa Mataifa, imesema kwamba bwana Onanga-Anyanga amepongeza wagombea Anicet Georges Dologuélé na Faustin Archange Touadéra, ambao wameongoza kwenye awamu hii ya kwanza ya uchaguzi iliyofanyika tarehe 30 mwezi uliopita.

Amewaomba kuendelea kuheshimu hali ya amani iliyotawala hadi sasa, na kuhamasisha pia wafuasi wao ili wawe na utulivu hadi mwisho wa mchakato wa uchaguzi.

Amekariri kwamba rais mteule atakuwa rais wa raia wote wa CAR.Halikadhalika Bwana Onanga-Anyanga amepongeza wagombea 28 wengine akiwaomba kuwasilisha malalamiko yao kupitia njia halali na kusihi wafuasi wao kuendelea kuwa watulivu.